Washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa klabu ya TP
Mazmebe ya Jamahuri ya Kidemokrasia ya Kongo wako shakani tena kujiunga
katika kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) iliyoanza kambi jijini Dar
es Salaam jana kutokana na uwezekano wa kuwekewa ngumu na timu yao.
Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa tayari wameshajulishwa
kwamba Samatta na Ulimwengu walioitwa kikosini na kocha wa Stars,
Mdenmark Kim Poulsen hawawezi kuungana na wenzao hadi shirikisho hilo
litakapozungumza na uongozi wa Mazembe ili kupata idhini ya kuwatumia.
Stars imeingia kambini jana kujiandaa kwa mechi tatu za kimataifa za kirafiki, ikiwamo dhidi ya timu ya taifa ya Ethiopia.
Wote wawili waliwahi kukataliwa na Mazembe kujiunga na timu ya taifa
ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyoshiriki michuano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) iliyofanyika
Kampala, Uganda na hivi karibuni walishindwa pia kuichezea Stars dhidi
ya Zambia baada ya kutua nchini wakitokea Kongo wakiwa majeruhi.
“Bado hatuna uhakika wa kuwapata Samatta na Ulimwengu… ila tumeanza
harakati za kuwaleta kitambo na tayari Sunday Kayuni (Mkurugenzi wa
Ufundi TFF) amekwenda Kongo kuwaombea ruhusa,” alisema Wambura.
Akieleza zaidi, Wambura alisema kuwa kambi ilianza jana na
kuwahusisha wachezaji wengine isipokuwa wa Simba, Azam na Mtibwa
zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi, Zanzibar na Yanga ambayo iko ziarani
Uturuki