LISSU AIBUA MAKUBWA:SEREKALI ITUELEZE KWANINI WAASISI SITA WA MUUNGANO WALIUWAWA NA KUZIKWA KABURI MOJA

Serikali imetakiwa kutoa maelezo bungeni, kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wanaodaiwa kuzikwa katika handaki moja Zanzibar.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza waasisi hao walifanya makosa gani.
Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama, Zanzibar.

Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu cha ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’ kilichoandikwa na Harith Ghassany alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika kaburi moja.

“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu huku wabunge wakiwa kimya kumsikiliza.
-Mtanzania
back to top