SHOGA, ABIRIA CHUNGA MZIGO WAKO IKIZIDI INAKUWA KERO

 
MMH! Nakuona mimacho imekutoka na kuangalia kama nitauanika ujinga unaofanya leo ndiyo hukumu yake. Kumbe unajua matatizo yako kwa nini usiyaache mpaka umsubiri Anti Naa niyaseme.
Jamani kona yenyewe ni finyu siwezi kuyasema yote kwa wakati mmoja, hebu acheni tabia chafu. Niwapeni siri za kudumu kwenye mapenzi pia kukufanya uyafurahie.
Leo nataka tuangalie wivu katika mapenzi, wote tunajua bila wivu hakuna mapenzi. Lakini wivu ukizidi unakuwa ugonjwa na vilevile kuwa karaha kwa mwenzako.
Kila kiumbe chenye akili timamu kilicho kamilika idara zote lazima kiwe na wivu. Kiumbe kisicho na wivu katika mapenzi ni sawa na mwili bila roho ambacho lazima kitakuwa ni maiti.
Lakini kwa kiumbe kinachovuta pumzi lazima kiwe na wivu na kama huna wivu na bado unavuta pumzi basi hujui kupenda. Lakini kwa yeyote anayeijua thamani ya kupenda lazima awe na wivu.
 Wivu ndiyo chachandu katika mapenzi kwa mtu kujua kweli anapendwa. Huwezi kuwa na mke au mume akichelewa au kusimama mazingira yasiyo eleweka ukae kimya. Mmh hapo lazima kuna walakini, siku zote abiria chunga mzigo wako ukiuacha ovyo utachukuliwa.
Lakini nataka kuzungumzia wivu uliovuka mipaka ambao huwa kero kwa wengine. Wapo wanaume au wanawake humuonea wivu hata mtu  akiwa na dada au kaka yake. Hamuamini mtu yeyote na kuamini unaweza kumfanyia kitu kibaya mpenzi wako.
Shoga zangu tunajua unampenda sana baba chanja wako, lakini lazima ujue unawezaje kupunguza  wivu ambao umekuwa kero kwa watu hata kuvunja uhusiano na watu kutokana na wivu wa kijinga.
Watu wa aina hii huamini wapenzi wao wakiwa mbali nao hakuna wanachowaza zaidi kufikiria ngono kila mara. Ukigundua hilo ujue una matatizo.
Wari wangu katika maisha kikubwa kusomana tabia,  mpaka mnakuwa pamoja mnakuwa mmeishajuana tabia zenu ili kuepusha presha zisizo na sababu. Kama mkiyarekebisha haya kila mmoja kuujua udhaifu wa mwenzie ambao unarekebishika basi mtakula raha bila karaha.
Hii si kwa wanawake tu hata midume mingine ina gubu hilo la kikwapa. Likirudi nyumbani lisimkute  mpenzi wake bila kujua labda amekwenda sokoni, dukani au kuteka maji hudhani amekwenda kwenye ngono. Kwa wanawake wenye wivu wa kijinga mumewe  amechelewa kazini hufikiri amepitia nyumba ndogo.  Jamani mbona tunaweza kuudhibiti wivu wa kijinga kwa kuitengeneza tabia ya wenzetu ambazo tunazijua vizuri, kitu kitakachofanya umjue vizuri mwenzako hata kutokuwa na wivu naye wa kijinga.
Ni kweli kila binadamu achunge mzigo wake, lakini ukizidisha huwa kero, peaneni uhuru ili  kuwafanya mfurahie maisha. Jamani eeh! Siyo basi ndiyo niwapeni mwanya kwa ajili ya kufanya uchafu wako kwa kusingizia kero za wenzenu, wengine kama nyani ukiwachekea utavuna mabua.
Jitambue kuwa wewe si mnyama ni mwanadamu unayetakiwa kujiheshimu, mwili wako anayetakiwa kuuthanifu ni mumeo au mkeo tu.
Usisababishe upuuzi wako uwanyime raha wenzako. Kama bado unataka kufanya uchafu wako usikubali kuingia kwenye uhusiano wa kujenga familia.
Kwa leo yanatosha, tukutane wiki ijayo ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.
chanzo; GPL.
back to top