Mwalimu Julius K. Nyerere.
KUNA siku Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere
aliwahi kusema “Ni mtu kichaa pekee, ambaye anaweza kufikiria kuipindua
serikali yangu au kujaribu kudhuru uhai wangu.”Mara baada ya kusema hayo wananchi kadhaa kwa kunong’ona walihusisha tambo hilo na nguvu za kishirikina wakiamini nguvu hizo zilimpa kinga. Na kweli aliweza kudumu madarakani muda mrefu, kwa kuheshimiwa na kuogopwa, pengine kuliko kiongozi yeyote aliyekuja kuongoza nchi hii baadaye.
Imani hii potofu inathibitishwa pia na watuhumiwa 19 wa kesi ya uhaini waliotaka kuipindua Serikali ya Mwalimu. Kesi hiyo ilidumu kwa miezi 10 na kumalizika Desemba 28, 1985; pale walipodai mahakamani kuwa, kama isingekuwa kile ‘kifimbo’ yaani uchawi wa Mwalimu, mpango wao wa kuipindua serikali, kati ya Juni 1982 – Januari 1983, usingebainika.
Kuwapo kwa kesi hiyo kulimaanisha kuwa Mwalimu Nyerere hiyo ilikuwa ni mara yake ya tatu kuko swakoswa kuuawa na wanajeshi. Ya kwanza ni maasi ya wanajeshi mwaka 1964, ya pili ni lile kundi la Bibi Titi Mohamed waliofungwa jela maisha mwaka 1970.
Mashitaka dhidi ya wanajeshi mwaka 1983 yalikuwa kwamba, wote kwa pamoja, kwa kushirikiana na raia mmoja, Bw. Pius Mtakubwa Lugangira, aliyekuwa akijulikana pia kwa majina bandia ya ‘Father Tom’ au ‘Uncle Tom walifanya uhaini.
Watuhumiwa hao ambao walifichuliwa njama zao na dereva teksi mmoja waliyekuwa wakimtumia mara kwa mara walidaiwa kuwa walikula njama kumuua Rais Nyerere, kumwondoa madarakani na kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Walikabiliwa pia na shitaka mbadala la kuficha kosa la uhaini kwa kushindwa kutoa taarifa kwa mamlaka inayohusika huku wakielewa juu ya mpango wa kuipindua serikali.
Itaendelea wiki ijayo.