Mazito yafichuka operesheni ya kimbunga nchini

Naibu Kamishna wa Polisi nchini na msimamizi wa operesheni kimbunga, Kamanda Simon Sirro akieleza jambo hivi karibuni. Picha ya maktaba 
  • Yabainika kuna wageni huja kuuza silaha
  • Operesheni hiyo imefanikisha pamoja na mambo mengine kukamata zaidi ya majangili 11 pamoja na meno ya kiboko na ngozi ya mbwea. Aidha jumla ya makokoro 12, bangi kilo tatu, gongo lita 271 na magunia ya mkaa 100 yaliyotengenezwa kwa mazao ya misitu kinyume na sheria vimekamatwa katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Hivi karibuni Serikali ilianzisha operesheni maalumu iliyopewa jina la ‘Operesheni Kimbunga’ kwa lengo la kuwaondoa nchini watu wote ambao hawana uraia au haki ya kisheria kuishi nchini.
Baadhi ya mambo mazito yaliyoibuliwa na operesheni hiyo ni kubainika kwa wahamiaji haramu ambao huja nchini kwa lengo la kufanya ujangili. Aidha wengine huja maalumu kwa lengo la kufanya ujambazi.
Kama hiyo haitoshi imebainika kwamba wapo ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kuuza silaha mbalimbali zikiwemo bastola na bunduki za aina mbalimbali zikiwamo Smg kutoka Burundi nan chi zingine. Wapo pia ambao huingia nchini kwa lengo la kulisha mifugo yao, na uthibitisho wa hili ni kwamba wapo ng’ombe kadhaa na mifugo mingine ambayo imekamatwan nchini ikiletwa kwa ajili ya kulishwa.
Operesheni hii ilikuwa na awamu mbili; ya kwanza ilianzisha Septemba sita hadi 20 mwaka huu na nyingine ya pili ni iliyoendelea ambayo ilianza Septemba 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani hivi karibuni, wahamiaji haramu 425 wamekamatwa wakiwamo wanaowahifadhi.
Ingawa baadhi ya watu wanailalamikia operesheni hii wakisema baadhi ya maofisa wanatumia mwanya huo kuwanyanyasa kwa kuwaondoa nchini watu wenye chuki nao, Serikali inasema haina ushahidi juu ya hilo na kwamba kama yuko mwenye kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali.
Kiongozi wa Timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa amesema opereshani hiyo haijaundwa kwa lengo la kumuonea yeyote wala kuwaondoa watu wa taifa fulani, bali kujua nani anaishi kwa haki na nani haishi kwa kufuata haki.
Anasema mpaka kufikia Septemba 20, 2013, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 9,283 toka nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Somalia, DRC Congo, Yemen na India, kwa madai ya kuishi nchini isivyo halali.
Kwanini kuna operesheni hii?
Zamaradi anasema kilichomsukuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuanzisha operesheni hiyo ni kukithiri kwa matukio ya uhalifu hasa katika mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi.
“Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo ujambazi wa kutumia silaha,ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafuagaji kutoka nchi jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho,” anasema Zamaradi.
Aidha amesema idadi kubwa ya wahamiaji haramu waliokamatwa ni kutoka Burundi (5,355) wakiafuatiwa na Rwanda (2,379), Uganda (939), DRC Congo (564), Somalia (44), Yemen (1) na India (1).
chanzo;Mwananchi.
back to top