WAREJESHA MENGI YALIYOKATALIWA NA CCM
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kukutana na viongozi wa vyama vyenye
wabunge kuzungumzia upungufu katika muswada wa marekebisho ya sheria ya
sheria mabadiliko ya katiba, viongozi wa vyama hivyo wametoa
mapendekezo mazito.Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa mapendekezo hayo mengi ni yale yaliyokataliwa na wabunge wa Chama Cha mapinduzi (CCM) wakati wakipitisha muswada huo bungeni.
Mapendekezo hayo ya wapinzani yanaonekana yatazua mtafaruku mkubwa bungeni iwapo serikali itaamua kuyapeleka, hasa baada ya Rais Kikwete kuwataka wapinzani kuandaa mapendekezo ya kina ya upungufu wa sheria hiyo na wayawasilishe haraka iwezekanavyo serikalini ili iunde kamati maalumu ya kujadili upungufu.
Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa viongozi hao wa vyama vya upinzani waliokutana Oktoba, 17, 2013 walijadili na kutoa mapendekezo kadhaa mbayo wameyawasilisha serikalini kama walivyoagizwa na Rais Kikwete.
Mapendekezo
Wapinzani hao wanapendekeza kifungu 22 (2A) cha sheria kama ilivyo sasa kifutwe kabisa, na kwamba wajumbe waliotajwa katika kifungu cha 22 (1) (c) watateuliwa na taasisi watakazowakilisha, na kwamba idadi ya wajumbe hao iongezeke kutoka 166 kwa mujibu wa sheria ya sasa hadi 438.
Wamependekeza kuwa makundi yote yanayostahili kuwakilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba yatafafanuliwa na idadi ya wawakilishi wao kuwekwa wazi katika jedwali la pili la sheria.
Pendekezo jingine linataka kuzingatia usawa wa kijinsia, kifungu kidogo (2b) kifutwe na kuandikwa upya “uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu chini ya kifungu kidogo (1) ( c ) utazingazia kanuni za sifa na zuoefu wa watu walioteuliwa, na idadi ya wajumbe wanawake haitapungua theluthi moja ya wajumbe walioteuliwa kutoka katika makundi hayo.”
Kwa kuzingatia dhana ya usawa wa wabia sawa wa Muungano bila kujali ukubwa wa kila nchi, idadi ya watu wake na kuzingatia haja ya kujenga muafaka na maridhiano ya kisiasa kuhusu muungano wetu, viongozi wa vyama, wamependekeza kama ilivyokuwa katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Katiba ya Mabadiliko ya Katiba, kutakuwa na uwakilishi sawa katika Bunge Maalumu kati ya washiriki wa Muungano.
Vile vile wamependekeza kuwa kifungu 22(1) kirekebishwe kwa kuongeza aya ya (d) isomeke “wajumbe wa Bunge Tume ambao hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika Bunge Maalumu yaani watakuwa wajumbe kwa nafasi zao ‘ex officio’ kwenye Bunge Maalumu.”
Hivyo kifungu (c) cha zamani za 37 (1) kirejeshwe ili kuwezesha uwepo wa tume hadi baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa, na idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu itakuwa 908, kwa mchanganuo wa 357 Bunge la Jamhuri, 81 Baraza la Wawakilishi, na 438 watakaoteuliwa na makundi tajwa katika kifungu 22(1) (c) na wajumbe 32 ‘ex officio’ wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia wamependekeza kwamba kifungu 26 (4) na (5) vifutwe badala yake kifungu (3) kirekebishwe ili kuweka wazi kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu wataendelea na majadiliano hadi kifungu husika kitakapoungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.
Mapendekezo hayo pia yamesema kwa jinsi sheria ilivyopitishwa kuzungumzia nafasi ya kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu sifa zake ni lazima mgombea awe na Shahada ya Chuo Kikuu kilichotambulika na uzoefu na ujuzi uliothibitika wa kuongoza mihadhara na mabaraza, kifungu hicho kitakuwa cha kibaguzi miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu ambao wengine hawajahitimu vyuo vikuu hivyo kukosa sifa ya kuteuliwa au kuchaguliwa.
Hata hivyo kwa kuwa kifungu hicho hakikutoa tafsiri ya neno mihadhara au mabaraza na mthibitishaji mwenyewe kutotajwa, wamependekeza kuwa mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu awe na sifa ya kugombea na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, na viongozi hao wachaguliwe badala ya kugombea.
Wapinzani wataka ushirikiano
Wakati Tanzania Daima Jumatano ikidokezwa kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo serikalini, viongozi wakuu wa vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UPDP, wametaka mchakato wa kupata katiba mpya ulenge maslahi mapana ya nchi na wananchi kuliko kufikiria maslahi ya vyama au makundi fulani katika jamii.
Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), James Mbatia alisema kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa katiba mpya, vyama vimedhamiria kuhakikisha kuwa mchakato wa katiba unafanyika kulenga maslahi mapana ya nchi.
“Sote kwa pamoja tunatambua tofauti mbalimbali ambazo ziko baina ya vyama vyetu kiitikadi na kimtizamo, lakini tunachukua jukumu kwa nia safi kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata katiba wanayoitaka,” alisema.
Vyama hivyo pia kwa tamko la pamoja vimesema vilikubali wito wa Rais Jakaya Kikwete alioutoa kupitia hotuba yake kwa Watanzania Septemba 4 na walipokutana naye Oktoba 5, mwaka huu, vimepongeza juhudi za rais kuhakikisha mchakato wa katiba unakwenda mbele ukihusisha wadau wote na wale walioachwa wasikilizwe kwa lengo la kuwaleta pamoja.
Mbatia alisema vyama vyao vinampongeza Rais Kikwete kwa nasaha zake kwa njia ya mazungumzo wakisema ni sahihi na ahadi ya kutoa ushirikiano mkubwa katika kila hatua ya mchakato wa katiba akiwa na lengo la kuona katiba inakuwa ya wote.
Kwa mujibu wa tamko hilo la TCD mkutano huo wa Ikulu na vyama sita vyenye wabunge na rais vilikubaliana kushirikisha vyama vingine 15 visivyo na wabunge kuandaa mapendekezo ya kina ya upungufu wa muswada ambao sasa umekuwa sheria na kupendekeza marekebisho maalumu na kuyawasilisha haraka iwezekanavyo.
Vile vile walipendekeza kuwa baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo serikalini ili serikali iunde kamati maalumu ya kukutana na vyama hivyo kujadili kwa kina juu ya upungufu katika sheria husika na kukubaliana juu ya maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho kwa lengo la kuufanya mchakato wa katiba kuwa shirikishi.
Mbatia alisema kulingana na makubaliano waliyofanya na rais, baada ya pande zote kukutana serikali itaandaa hati ya dharura ili sheria husika irejeshwe bungeni haraka katika mkutano wa Bunge unaoanza wiki ijayo.
Alisema kuwa katika mjadala wa kitaifa, taasisi mbalimbali katika umma, makundi ya kijamii na wadau wote muhimu wahusishwe ili kutengeneza maridhiano ya kitaifa.
Mbatia alitoa wito kwa niaba ya vyama vyote vya siasa kuwaomba Watanzania wote hususani wabunge waunge mkono juhudi hizo za vyama na Rais Kikwete kuhakikisha mchakato wa katiba mpya unakuwa shirikishi utakaolinda maslahi mapana ya taifa.
Tamko hilo lililosomwa na Mbatia lilikuwa limesainiwa na Philip Mangula (CCM), Freeman Mbowe ambaye aliwakilishwa na Dk. Slaa (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema aliyewakilishwa na Nancy Karia (TLP), John Cheyo aliyewakilishwa na Isaac Cheyo (UDP) na Fahmi Dovutwa wa UPDP kwa niaba ya vyama visivyo na wabunge.
Mangula agoma kuisema CCM
Baada ya tamko hilo, wakati wa maswali, waandishi walitaka kujua kauli ya CCM kwani wamekuwa wakisisitiza kuwa mchakato huo ulikuwa huru na ulipitia hatua zote, kama wapo tayari kufanya mabadiliko kama alivyopendekeza rais na vyama vyenye wabunge.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula aligoma kuzungumza kwa undani na kusema: “Mimi sio mbunge siwezi kuwasemea wabunge.”
Kauli hiyo ilisababisha Mbatia kuanza upya kuwataka waandishi na Watanzania waache tofauti zao, waache kauli zote zilizowahi kutolewa na kutoa fursa mpya ya kuanza mchakato kwa njia ya amani kwa maslahi mapana ya taifa.