KESI YA BILIONEA WA MADINI...


Ile kesi ya mauaji ya aliyekuwa bilionea, mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite jijini hapa, Erasto Saimon Msuya (43) imeahirishwa hadi Desemba 11, mwaka huu huku kukiibuka maajabu au sintofahamu mahakamani kufuatia watu kuzimia na kupigwa upofu.


Katika kesi hiyo iliyosomwa kwa mara nyingine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mapema wiki hii, mara tu baada ya kuahirishwa kesi hiyo ndipo baadhi ya watu wakazimia akiwemo mdogo wa marehemu Erasto.
Katika hali ya kushangaza, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mbali na watu kuzimia, wapo waliodai kupigwa upofu ambapo wote kwa pamoja walikimbizwa hospitalini.
Baadaye walielezwa kurudi kwenye hali zao za kawaida.
Kesi hiyo inahusisha watuhumiwa nane ambapo mtuhumiwa namba tano, Joseph Damas Mwakipesile ‘Chusa’ (34) akishirikiana na Ally Musa ‘Majeshi’ na wengine sita walidaiwa kummiminia risasi zaidi ya 20 na kumuua bilionea huyo.
Wengine sita ni Sharif Mohamed Athuman (31), Shaibu Jumanne Saidi ‘Mredi’ (38), Jalila Zuberi Said (28), Sadick Mohamed Jabir ‘Msudani’ au ‘Mnubi’ (32), Karim Kihundwa (33) na Mussa Juma Mangu (30).
Watuhumiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kuhusika na mauaji ya Bilionea Erasto yaliyotokea Agosti 7, mwaka huu kandokando ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, eneo la Mjohoroni wilayani Hai karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
back to top