
Wagonjwa wakiwa wamepumzika katika mazingira duni sana ndani ya moja ya
zahanati za umma zilizoko maeneo ya vijijini. Wengi wako katika hatari
kubwa kwani uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha mfumo mzima wa kitabibu
Tanzania umeoza, huku wagonjwa wakitumbukia katika makucha ya madaktari
na wafamasia feki, wanaotoa vipimo visivyofaa, na dawa zisizokidhi
viwango.Baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu kwenye
maduka wanawauzia wateja wao dawa tofauti na zile walizoandikiwa kwenye
vyeti na madaktari kwa maelezo kuwa walizonazo ni bora zaidi au ni za
aina moja ila zimetengenezwa na viwanda tofauti.
Wiki
iliyopita tuliona ushuhuda wa daktari feki aliyejitambulisha kwa jina la
Ramla Maganga (siyo jina lake halisi), akieleza namna alivyokuwa
akihudumia wagonjwa kwenye zahanati binafasi wilayani Temeke, Dar es
Salaam. Inaendelea…
Madhara yatokanayo na madaktari feki
Daktari bingwa wa upasuaji, Hospitali ya Aga Khan,
Dk Aidan Njau anasema madaktari feki wanasababisha madhara makubwa kwa
wagonjwa kwa kuwa wanatumia uzoefu badala ya taaluma ya matibabu.
“Hawa watu wanatoa dawa kwa mazoea, baadhi yao
wamefanyakazi wodini kama manesi kwa miaka 10 hadi 20 wakiwaona
madaktari wanavyotoa dawa. Wengine wamefikia hata hatua ya kuwa na
vibanda vya dawa mitaani,” alisema.
Anasema kwamba baadhi ya madaktari hao huwapa
wagonjwa dawa chini ya kipimo kinachotakiwa, hivyo kuwafanya washindwe
kupona, huku wengine wakizidisha dozi na kusababisha madhara kwenye
maini na figo.
“Wanatoa dawa bila kufanya vipimo. Mgonjwa anapewa
dawa ya maumivu anameza, baada ya mwezi anagundulika kuwa ana saratani.
Mtu mwingine anasema anasikia maumivu tumboni anapewa dawa ya maumivu,
kumbe ni Appendisitis (shambulizi la kidole tumbo) baadaye kinapasuka.
Mbaya zaidi baadhi yao wanauza dawa zilizokwisha muda wake,” anasema.
Maduka ya dawa yanauza dawa tofauti
Baadhi ya wauzaji wa dawa za binadamu kwenye
maduka wanawauzia wateja wao dawa tofauti na zile walizoandikiwa kwenye
vyeti na madaktari kwa maelezo kuwa walizonazo ni bora zaidi au ni za
aina moja ila zimetengenezwa na viwanda tofauti.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye maduka
kadhaa ya dawa muhimu, umebaini kuwa baadhi ya wauzaji kwenye maduka
hayo huwalazimisha wateja wao kununua dawa tofauti ambazo hazina uwezo
wa kutibu ugonjwa husika.
Mwandishi wetu alitumia cheti cha mgonjwa
aliyeandikiwa dawa aina ya Clarithromycin kuzunguka kwenye maduka
mbalimbali ya dawa, lakini kila alipokwenda aliuziwa dawa zenye majina
tofauti huku akiambiwa kuwa zote zinatibu ugonjwa ya aina moja.
Katika duka la kwanza lililopo Mbagala Kuu,
wilayani Temeke, muuzaji ambaye hakufahamika jina lake, alipoulizwa kama
ana dawa ya Clarithromycin alijibu kuwa anayo. Hata hivyo, alileta dawa
aina ya Erythtromycin na kumkabidhi mwandishi bila maelezo yoyote.
Alipoulizwa mbona dawa hiyo ni tofauti na ile
aliyoandika daktari, muuzaji huyo alisisitiza kuwa zote zina nguvu sawa
ila zimetengenezwa na kampuni tofauti.
-MWANANCHI
-MWANANCHI