Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’
KWAKO,Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ Mdogo wangu, nimekufuatilia tangu mwanzo kabisa wakati ukianza kurusha kete yako ya kwanza kwenye game. Niliuona uwezo wako, nikajua kweli una kitu fulani kwenye burudani.
Ulikuja na staili ya peke yako kabisa lakini lazima nikuambie ukweli, ilikuwa staili ambayo ilihitaji sana sapoti ya mtu mwingine. Kama ungetoka kivyakovyako, kidogo kungekuwa na mawaa katika kutoka. Tip Top Connection wakaamua kwa moyo mmoja kufanya kazi na wewe – ukang’aa.
Kabla sijaenda mbali zaidi nataka kukukumbusha kwamba, wapo vijana wengi sana mitaani (hata Arusha ambapo unatokea) lakini hawajulikani. Si ajabu wana uwezo mkubwa zaidi yako na wanatamani kupata nafasi ya kutoka lakini hakuna anayewafahamu.
Nyota yako imeng’aa umekubalika na kaka zako ambao wamependa kufanya kazi na wewe. Lazima utulize kichwa, nidhamu ya hali ya juu na ubunifu mkubwa ndipo utaweza kuendelea kuwa matawi ya juu, vinginevyo utadondoka!
Nilifuatilia sakata lako na Hamadi ‘Madee’ Ali, Kiongozi wa Tip Top Connection baada ya kushindwana naye na akaamua kukurudisha nyumbani kwenu Arusha. Wengi walikuwa upande wako, wakayasadiki uliyosema, kwamba bwana mkubwa huyo alikuonea na kukunyanyasa na kukupa fedha ambazo hazikulingana na kazi unayofanya.
Muda mfupi tu baadaye, Watanashati Entertainment ya Ostaz Juma Namusoma, wakaamua kukuchukua na kurekebisha kila kitu kuhusu maisha yako ya kisanii. Wiki iliyopita, yakaibuka mapya.
Ikaelezwa umetimuliwa kwa kosa la utovu wa nidhamu na kukataa shule pamoja na mambo mengine. Nikajiuliza; huyu mtoto ana nini? Sikukupatia picha. Kosa alilolisema Ostaz ni lilelile alilowahi kusema Madee.
Nikajiuliza; hawa watu wanaambiana? Iweje wote wakushutumu kwa kosa moja? Ukifuatilia vizuri, utagundua kwamba, makosa yanayowatofautisha ni kwa faida yako mwenyewe mdogo wangu. Suala la nidhamu ni la maisha yako.
Mtu anayesimamia mahudhurio yako shuleni ni mtu mwema kwako, maana anayaangalia maisha yako mbeleni nje au ndani ya muziki. Ni mtu mwenye lengo jema nawe. Nini kinachok-usumbua dogo? Ni umaarufu? Starehe au nini?
Nimefurahi kusikia kwamba mmeshaweka mambo sawa na umerudishwa kundini lakini nakusihi mdogo wangu, tuliza kichwa chako. Chagua marafiki wema. Kukaa chini ya uangalizi ni kitu kizuri kwa maisha yako.
Umri wako bado mdogo, hujafikia kiwango cha kuwa na maamuzi yako kwa kila kitu. Unahitaji muongozo. Sanaa bila elimu ni kazi bure. Kama umepata nafasi ya kusoma, piga kitabu, tena uwe na malengo ya mbele zaidi ya kuendelea na chuo.
Usiende shule kwa lengo la kumfurahisha mtu, bali ujue unatengeneza maisha yako ya baadaye. Achana na mambo mengine kwa sasa, elekeza akili yako katika kubuni vitu vipya. Hebu mwangalie mwenzako Diamond (Nasibu Abdul), yupo juu kimuziki.
Hajawahi kutetereka tangu ameanza. Unajua kwa nini? Kwa sababu ni mbunifu. Achana na usela usio na maana, angalia wanachokitaka mashabiki kisha uwapatie. Una kazi kubwa sana ya kurudisha imani kwa mashabiki wako.
Jifunze kutoka kwa wenzako. Heshimu mamlaka inayokuongoza. Kwa bahati nzuri, wazazi wako wapo karibu na wewe na wanafuatilia sana maendeleo yako ya kimuziki na maisha kwa jumla. Ni jambo la kujivunia sana.
Waswahili wana msemo wao usemao; “Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu!” sasa kazi kwako kuamua kuishi kwa nidhamu na kuongeza ubunifu au kuendelea na mambo yako kama akili yako inavyokuongoza. Chukua yanayokufaa yafanyie kazi, pumba ziache hapahapa.