AAAH HEMED PHD, UNALAZIMISHA UNYAMWEZI?

 
Hemed Suleiman 'PHD'.
JINA lake halisi ni Hemed Suleiman, lakini mwenyewe aliamua kutumia la kisanii, ambalo limemkaa vyema kama PHD. Ni mmoja kati ya wasanii chipukizi lakini waliojipatia majina makubwa katika burudani Tanzania.

 
 Binafsi namfahamu kuanzia wakati wa Shindano la Tusker Project Fame, Season 2 lililofanyika Nairobi nchini Kenya mwaka 2008. Nilikuwa mmoja wa wadau waliokuwa wakifuatilia kwa karibu shindano lile na bado nakumbuka jinsi kijana huyu, mwakilishi wa Tanzania alivyotoa machozi baada ya kuibuka kwa Ambwene Yessaya ‘AY’ jukwaani siku ya fainali, akiwa kama msanii mkubwa kutoka nje kuja kutumbuiza mbele ya washiriki.
Hemed alitoa machozi kumwona staa kutoka nchini kwake akiwa mmoja ya wasanii wakubwa wanaotumbuiza jukwaani siku hiyo. Kwake ilikuwa ni surprise kwa vile wakati huo, AY alikuwa zaidi ya mlima Kilimanjaro.
Ingawa hakuchukua nafasi ya kwanza katika shindano lile, lakini kipaji chake kilijionyesha wazi na ndiyo maana aliporejea tu Bongo, akajikita katika muziki na baadaye filamu!
Nimemuona akicheza muvi kadhaa. Ingawa yeye binafsi anaweza akipata ‘director’ mzuri, lakini bado nasisitiza kuwa filamu nyingi za hapa nyumbani zinatengenezwa kwa kulipuliwa sana, hazina ubora, zinakosa mtiririko na mbaya zaidi, waigizaji wetu wanajua zaidi kuliko uwezo wao.
Kwangu, PHD ni maarufu zaidi kuliko nyimbo au filamu zake. Huenda kwa vile hamu ya kusikiliza muziki na kutazama filamu inashuka kila siku kutokana na waburudishaji wetu kukosa ubunifu mpya.
Ninajisikia ku-enjoy zaidi kusikiliza kazi za watu kama Sugu, Profesa Jay, Mr Nice, Inspekta Haroun, Juma Nature, AY, FA, Lady Jay Dee, East Coast, Wateule, Ray C, Gangwe Mob, Stara Thomas na wenzao wa enzi hizo kuliko hawa wa sasa.
Na sijui nikoje, nadhani ninapata burudani na kujifunza zaidi nikitazama marudio ya maigizo ya makundi kama Mambo Hayo, Kidedea na Kaole kuliko waigizaji wa filamu wa Dot.com waliojazana sasa.
Nimewahi kusikia vioja vingi vya PHD. Ameshawahi kutamba kuwa yeye anababaikiwa sana na wanawake, kuna kipindi pia alikwaruzana na muigizaji mwenzake, Yussuf Mlela hadi kufikia kutambiana nani mzuri kati yao!
Kubwa zaidi, huyu ‘bwa mdogo’ aliwahi kuandika katika moja ya kurasa zake za mitandao ya kijamii akisema yeye ni shoga. Baada ya watu kumshambulia, alitoa utetezi dhaifu kwamba eti alisema vile kwa kuwa alitaka kuona wasichana aliotembea nao, aliodai wanafikia 32, watajisikiaje!
Nimeiona video ya wimbo wake mpya, uitwao The Rest of My Life. Nadhani ni moja kati ya video nzuri na za kisasa kwa kiwango cha Bongo. Lakini kuna jambo ambalo kama wadau, lazima tujaribu kumshauri kwa manufaa ya maadili ya kizazi chetu.
PHD amemchukua mwanadada aliyemfanya kama Video Queen wake, akamchezesha uchi. Amevaa chupi na sidiria tu, utafikiri unatazama video ya Rihanna.
Si aina ya video zinazotengenezwa kwa ajili ya Watanzania zinazopaswa kurushwa. Hata kama msanii huyu anatafuta soko la kimataifa, ni lazima tuenzi utamaduni na maadili yetu kama taifa. Najaribu kushangaa, wakati kuna chombo cha kukagua filamu baada ya malalamiko mengi, vipi kile cha kukagua video za wasanii hawa?
Katika akili ya kawaida, wateja wakubwa wa kazi za Hemed ni Watanzania, ambao ni vigumu kutazama video hiyo wakiwa na familia, hata kama tunajidanganya kwamba tunakwenda na wakati.
Anapenda Unyamwezi (Umarekani), lakini sidhani kama hapa ni mahala pake. Wasanii ni kioo cha jamii, hili tunalisema kila mara, tunao watoto wanaotamani kuwa kama wao ukubwani mwao, tunawafundisha nini?
PHD na staa mwingine ye yote anaweza kuwa Mnyamwezi akiwa Club, lakini anapofanya kazi za kuwapelekea wateja wake, lazima atambue kwamba walaji wake ni jamii ya Kitanzania, inayohitaji malezi ya Kitanzania!
back to top