
Mafaili na makabrasha yanayotumika kutunza kumbukumbu mbalimbali
“Nilipowasili Tanzania Septemba mwaka jana,
nilikutana na maswali mengi, kubwa lilikuwa kuhusu uchumi wa Korea,
hasa namna ambavyo umekuwa haraka,” hayo ndiyo yalikuwa maneno ya
ufunguzi wa semina yaliyotolewa na balozi wa Korea Kusini hapa nchini
wiki iliyopita.
Balozi huyo Chung Il, anasema mara kwa mara
waandishi wa habari wamekuwa wakimuuliza hatua gani ambazo Korea
ilizichukua na kuiwezesha kuwa moja ya nchi tajiri duniani wakati miaka
ya 1960 ilikuwa ikilingana na Tanzania kiuchumi.
“Waandishi huniuliza, miaka ya 1960 Tanzania na
Korea zilikuwa na hali sawa ya kimaisha, kwa kuwa na pato sawa. Siku
hizi kuna tofauti kubwa sana nini siri yake?” anasema Il.
Il anasema anawajibu kwa kuwaambia mafanikio ya
kiuchumi ya nchi yake siyo muujiza bali ni matokeo ya umakini na roho ya
kuthubutu iliyoungwa mkono na mwelekeo wa soko huria duniani.
Korea ambayo ‘ilijichomoa’ mikononi mwa ukoloni wa
Japan mwaka 1948, imefanikiwa kuongeza pato lake la mauzo ya bidhaa nje
kutoka Dola 41 milioni za Marekani mwaka 1961 hadi Dola 548 bilioni za
Marekani mwaka 2012. Huku umri wa kuishi ukiongezeka kutoka miaka 55.3
hadi miaka 81.2.
Siri ya Korea Kusini
Pamoja na mafanikio hayo, Balozi Il anasema
hakubaliani na njia ya kukuza uchumi iliyotumiwa na viongozi wa taifa
hilo katika miaka ya 1970 na 1980 kwa kuwa zilibomoa utamaduni wa asili
ya Mkorea.
“Sasa kuna mambo mengi ya kijamii yasiyofaa
yanafanyika, wanauchumi na vyama vya wafanyakazi wanajaribu kutatua
matatizo ambayo ni matokeo ya miaka ya 1970 na 1980,” anasema Il.
Il alikuwa akizungumza jijini Dar es Salaam katika
semina iliyopewa jina ‘Siri ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Korea’
iliyoandaliwa na Ubalozi wa Korea nchini kwa kushirikiana na Taasisi ya
Utafiti ya Kuondoa Umasikini (REPOA).
Semina hiyo ambayo ililenga kujadili namna ambavyo
maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa na Korea yanavyoweza kuisaidia
Tanzania, ilihudhuriwa na wataalamu mbalimbali wa uchumi.
Msemaji mkuu katika semina hiyo, Mkuu wa Chuo cha
Maendeleo cha Korea (KDI), Dk Sang-woo Nam anasema kuwa Rais Park Chung
Hee aliyeiongoza Korea kati ya mwaka 1961-1979 aliweka ahadi ya kuwatoa
wananchi kwenye umasikini.
Nam anasema rais huyo aliweka mipango ya miaka
mitano ya maendeleo ya kiuchumi huku akipambana na rushwa na kuwa na
mikutano kila mwezi akifuatilia hali ya maendeleo ya kiuchumi.
chanzo;mwananchi.
chanzo;mwananchi.