
Spika Makinda alishangazwa na Mtanzania
anayeshindwa kupata Sh1,000 kwa mwezi, kufafanua kuwa kama wananchi
wataifanya nchi yao kuwa rahisi, watalalamika na umaskini mpaka siku
watakayokufa. Julai 30 mwaka huu, Waziri wa Fedha, William Mgimwa
alikaririwa akisema suala hilo litamalizwa bungeni kisheria na kwamba
wameanza kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuitaka Wizara ya
Fedha kukutana na wadau wengine, kuangalia namna ya kupata vyanzo
vingine vya mapato mbadala na kodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya
ufunguzi wa mafunzo ya wajumbe wa kamati ya Hesabu za Serikali Kuu
(PAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti, Spika Makinda
alisema, “Haya maendeleo tunayoyataka sisi kama Watanzania yatapatikana
kwa kulipa kodi, hata vitabu vitakatifu vinasema kila mtu lazima
achangie,”alisema.
Alisema bila kukusanya kodi nchi itashindwa
kujiendesha na kusisitiza kuwa kama angeulizwa kuhusu masuala ya
ulipaji kodi angesema uanzishwe hata mfuko maalumu wa kuwasaidia vijana.
Alisema kwa kuwa suala hilo la kodi hivi sasa ni
sheria, mabadiliko yake ni lazima yarudi bungeni na kwamba haamini
katika kushindwa kulipa fedha hiyo.
“Tunataka kufanya vitu vingi na hatuwezi
kuitegemea Serikali katika kila kitu sasa yenyewe itatoa wapi fedha.
Hayo ni maoni yangu lakini hiyo ni sheria,” alisisitiza Spika Makinda.