MWANAFUNZI wa kidato cha pili jina kapuni (16), amejikuta akiozeshwa na
wazazi wake kwa mwanaume aliyetambulika kwa jina la Kaizilege Jabiri
(31) ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa, Risasi Mchanganyiko linakupa
habari.
Tukio hilo lilitokea Juni 14, mwaka huu jijini Dar nyumbani
kwao Mlandizi, Bagamoyo, Pwani ambako mwanaume huyo alifunga ndoa na
binti huyo na kurejea naye nyumbani kwake, Ubungo Kisiwani, Dar huku
baadhi ya watu wakihofia uhai wa ndoa hiyo.
Baada ya kuanza maisha ya
ndoa kama mke na mume, Agosti 6, mwaka huu taarifa zikafika kwenye
Kituo cha Polisi cha Ubungo ambapo maafande walisema hiyo haiwezekani.
“Polisi walipopata habari walisema hakuna ndoa hapo, wakajipanga kwenda kuvamia nyumbani kwa wanandoa hao,” kilisema chanzo.
Chanzo
kiliongeza kuwa, nje ya nyumba hiyo walimkuta msichana huyo anapika
huku kaka yake akiwa kajipumzisha ndani akisubiri lishe hiyo.

Kaizilege
alipobanwa alikiri kuwa mwanafunzi huyo ni mkewe walifunga ndoa ya
Kiislamu, Mlandizi. Kwa kuwa kisheria ni kosa kuoa mwanafunzi aliye
chini ya miaka 18 alilazimika kupelekwa Kituo cha Polisi, Magomeni, Dar.

Kwa
upande wake mwanafunzi huyo alikiri kuolewa na kaka yake. Alisema yeye
ni mwanafunzi, yuko kidato cha pili Mlandizi. Alisema hakuwa na maamuzi
ya kuikataa ndoa hiyo kwani uwezo huo ni wa wazazi wake.
Denti huyo
alizidi kuweka wazi kwamba, chanzo kikubwa cha kuozeshwa kwake ni
kutokana na ugumu wa maisha ulioko katika familia hali iliyomsukuma baba
yake mzazi kumshawishi aolewe na kaka yake.
Alisema kuwa aliambiwa atakapoolewa, mumewe huyo angeendelea kumsomesha jambo ambalo halikufanyika.
‘’Mimi
nilikubali niolewe ili baadaye nipelekwe shule kwani wazazi wangu
hawana pesa za kunisomesha na mimi siwezi kukataa kwa sababu wazazi
ndiyo wameamua,’’ alisema.
VYANZO VYA HABARI
Hata hivyo, kwa
mujibu wa baadhi ya ndugu, dini ya wawili hao inaruhusu kumuoa mtoto wa
mama’ke mkubwa endapo atakuwa amefikisha umri wa miaka 18 haki ambayo
kwa mwanafunzi huyo haipo.
Risasi Mchanganyiko liliwasiliana na
msemaji wa dawati la jinsia Wilaya ya Kinondoni, Dar, Inspekta Prisca
Komba ambapo mhusika mmoja alisema:
‘’Kwa mujibu wa sheria na
taratibu za utamaduni wetu si ruhusa kuoa mtoto wa mama mkubwa tena
akiwa bado mwanafunzi, mimi naona ni kuvunja sheria na ni lazima huyu
bwana afunguliwe jalada la uchunguzi.”
Kaizilege amefunguliwa jalada
la uchunguzi kwa Kumbukumbu MAG/RB/9015/2013, mara uchunguzi
utakapokamilika atafikishwa mahakamani.