Jacob Stephen Mbura ‘JB’.
Jacob Stephen Mbura ‘JB’. Habari za
masiku mtu mzima. Kitambo kidogo hatujaonana kaka. Hata hivyo, leo
nimeona nikukumbuke kwa barua.Kiukweli kwa muda mrefu sana nimetafakari kuhusu kukuandikia hii barua au kuacha. Changamoto zilikuwa nyingi kichwani mwangu lakini pengine kubwa zaidi ni kutokana na jamii inavyokuheshimu (nikiwemo mimi) na kuamini kwamba upo katika levo za juu sana kisanii.
Hilo lina ukweli lakini nahitaji kukumbusha jambo moja la muhimu. Pamoja na uwezo wako mkubwa wa kuigiza na namba kubwa ya mashabiki uliyonayo hivi sasa, uko hatarini kuporomoka au inawezekana ukabaki katika levo hiyohiyo jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
Uwezo wako ni mkubwa na unaweza kufanya zaidi ya hapo. Zipo kasoro ninazoweza kuziita ndogondogo ambazo kwa hakika kama ukizifanyia kazi, utazidi kuwa juu kwenye game na itakuwa vigumu sana kwa wasanii wengine kukufikia.
Ngoja nikumegee siri, kwa vipaji ninavyoviona hivi sasa, kuna hatari sana ya kuchukua nafasi yako kama hutashtuka na kuendelea kuamini kuwa wewe ni namba moja na utaendelea kubaki hivyo.
Kwa leo sitakutajia orodha ya wasanii chipukizi ambao wanakuja kwa kasi ya moto wa kifuu ambao kwa hakika wanatishia kukunyang’anya ufalme.
Sina tatizo na uigizaji wako wala kuvaa uhusika, kasoro ninazoziona ni hizi zifuatazo ambazo zinahitaji marekebisho ili uendelee kuwa juu na kuvuka mipaka ya nchi yetu.
KICHEKO
Wakati mwingine, msanii anaweza kuona anapatia sana katika uhusika fulani na akajisahau na kujikuta kila sinema anarudia kitu hichohicho bila kujali kuwa kwa namna moja ama nyingine kinawaboa watazamaji wake.
Suala la kicheko kwako imekuwa kama nyanya kwenye mchuzi! Kuna mahali pengine hapahitaji kicheko lakini lazima ucheke tena katika kiwango cha ‘uigizaji’ kiasi kwamba mtazamaji anajua kabisa anaibiwa!
STORI
Hapa nitakuzungumzia wewe kama mtayarishaji wa sinema ambaye una kampuni yako ya Jerusalem. Kwa hivi karibuni, stori zako zimekuwa kama zinafanana tu kwa sababu utakuta visa vinakaribiana au maana inakuwa moja.
Umekuwa ukicheza zaidi sinema zenye hadithi za mapenzi na wewe ukionekana kama ‘kidume’ ambaye una ‘tekiniki’ za kutosha katika mapenzi. Hili ni tatizo.
Jaribu kuchanganya hadithi hasa kwa sababu kama mtayarishaji una uhuru wa kuamua na kuchagua stori nzuri ambayo haiwezi kuendana wala kukaribiana na zilizotangulia.
Ili kukuthibitishia hili, angalia Filamu za Regina, Dereva Teksi, Vita Baridi, Ukurasa Mpya, Fikra Zangu, Zawadi Yangu, Zawadi ya Birthday na Dj Ben zinaweza kuwa mfano wa ninachokizungumzia hapa.
ANGALIA TOFAUTI
Ili uone kuwa inawezekana kuvaa uhusika tofauti na bado ukacheza vizuri zaidi, angalia katika sinema ambazo umeshirikishwa nje ya kampuni yako. Nyingi umecheza katika uhusika tofauti kabisa.
Mifano mizuri ni katika filamu kama Tanzanite, Well Done My Son, Shakira, Offside, I Think I Hate My Wife na nyingine nyingi.
Mtu mzuri ni anayekuambia ukweli. Kusifiwa umejenga nyumba nzuri wakati inaonekana ina nyufa hakuna maana kwa sababu baada ya muda itaanguka na atakayebaki na masikitiko bado utaendelea kuwa ni wewe.
Ukweli ni mzuri lakini wakati mwingine unauma. Ukiona maneno yangu yana maana yafanyie kazi, ukiona ni stori kama za Mpekepeke, acha hapahapa.
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa,
Mumbai, India.