
Samuel Eto’o huenda akaungana na Mourinho kwa mara nyingine.
Mshambuliaji
wa timu ya taifa ya Cameroon Samuel Eto’o huenda akaungana na kocha
wake wa zamani Mreno Jose Mourinho baada ya kuweka wazi utayari wake wa
kujiunga na Chelsea endapo nafasi hiyo itajitokeza.
Eto’o
amewekwa kwenye orodha ya wachezaji wanaotarajia kuuzwa na klabu ya
Anzhi Makhachkhala ya Urusi baada ya bosi wa klabu hiyo kubadili sera ya
usajili toka kwenye kusajili wachezaji nyota wenye majina makubwa na
wanaolipwa mishahara minono na kuamua kujenga timu yenye wachezaji wa
bajeti ya chini.
Kwa
muda wa miaka miwili Eto’o amekuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi
kuliko wote duniani baada ya kukubali kujiunga na Anzhi ya Urusi
akitokea Inter Milan ambako alicheza kwa miaka miwili baada ya kuondoka
Barcelona.
Kundi
la wachezaji raia wa Urusi wakiongozwa na nahodha wa timu ya taifa hilo
Igor Denisov walianzisha mgomo baridi ndani ya kambi ya Anzhi
Makhachkhala dhidi ya wachezaji wageni wanaolipwa fedha nyingi kama
Eto’o hali ambayo imesababisha mwenyekiti wa timu hiyo kubadili sera ya
usajili na uendeshaji wa timu hiyo.
Sambamba na Eto’o, staa kama Lassana Diarra, Lacina Traore, Christopher Sambana wengineo wanatarajiwa kuuzwa kwa timu zinazowahitaji.
Kwenye
sentensi nyingine ni kwamba siku kadhaa zilizopita Anzhi ilitangaza
kumfukuza kazi kocha wake Rene Meulenstein ambaye alikuwa amekaa na timu
hiyo kwa mwezi mmoja pekee akiwa amekuwa kocha mkuu kwa muda wa siku
kumi na sita baada ya kushika nafasi hiyo kufuatia kujiuzulu kwa kocha
Guus Hiddink.

Mgawanyo wa mshahara anaopata Eto’o ndani ya klabu ya Anzhi Makhachkhala.

Eto’o anaongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa kuliko wachezaji wote duniani.
Eto’o
mwenyewe ameonekana kuvutiwa na uwezekano wa kuungana na kocha wake wa
zamani ambaye walifanya kazi kwa mafanikio ndani ya Inter Milan ambapo
klabu hiyo ilitwaa mataji matano katika kipindi cha misimu miwili.
Chelsea
itamsajili Eto’o endapo itashindwa kumsajili mshambuliaji wa Manchester
United Wayne Rooney ambaye Mourinho amemtangaza kuwa chaguo lake namba
moja kwenye usajili wake.