
Dar
es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeiamuru Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu iwasilishe majalada ya kesi ya ugaidi inayomuhusu
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na
mwenzake katika kesi hiyo, Ludovick Joseph.
Hati
ya kuitisha majalada hayo ilitolewa jana alasiri na Msajili wa Mahakama
Kuu, baada ya mawakili wanaomtetea Lwakatare kuwasilisha maombi ya
marejeo ya mwenendo wa kesi hiyo, iliyofunguliwa katika Mahakama ya
Kisutu.
Maombi
hayo ya marejeo yaliwasilishwa mahakamani hapo jana chini ya hati ya
dharura yakiambatanishwa na hati kiapo ya mmoja wa mawakili wanaomtetea
Lwakatare, Peter Kibatala. Wengine ni Mabere Marando, Profesa Abdallah
Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu.
Habari
ambazo gazeti hili lilizipata kisha baadaye kuthibitishwa na mmoja wa
mawakili wanaomtetea Lwakatare zilisema kuwa jana Msajili wa Mahakama
Kuu alisaini na kutoa hati hiyo kwenda Mahakama ya Kisutu.
Mapema jana mawakili wanaomtetea Lwakatare waliwasilisha maombi hayo ambayo yalipokewa na kupewa usajili wa namba 14 ya 2013.
Mawakili
hao wanaiomba Mahakama Kuu, iitishe majalada yote mawili ya kesi hiyo,
jalada namba 37 ya mwaka 2013 na namba 6 ya mwaka 2013 kwa ajili ya
uchunguzi ili iweze kujiridhisha usahihi na uhalali wa mwenendo wake.
Pia
wanaiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo na/au kutengeua hati ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyowafutia mashtaka watoa maombi (Nolle
Prosequi) kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayohayo.
Maombi
yao mengine ni kutaka Mahakama ya Kisutu iamriwe kutoa uamuzi wa maombi
ya dhamana, uliokuwa umepangwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi,
Emillius Mchauru, Machi 20, 2013, katika kesi namba 37.
Mawakili
hao wanadai kuwa uamuzi huo ambao ulihusu dhamana ya watuhumiwa,
ulitenguliwa na hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka washtakiwa hao, isivyo
halali.
Maombi
mengine ni kurejea na/ au kutengua mwenendo wa kesi namba 6
iliyofunguliwa baada ya hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi hao na
badala yake iendelee kesi namba 37.
Wanaiomba
pia Mahakama Kuu iamue kwamba utaratibu uliotumiwa na wajibu maombi
(Jamhuri) kutoa hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi katika kesi
namba 37 ilikuwa kinyume cha sheria na/ au haukuwa sahihi.
Wanadai
kuwa utaratibu huo ulisababisha matumizi mabaya ya taratibu za
kimahakama na matumizi mabaya ya mamlaka ya kiuendeshaji mashtaka na
kushusha hadhi na uhuru wa mahakama.
Chanzo: Mwananchi