Nchemba aandaa hoja kujadili mikopo ya elimu ya juu nchini

Mbunge wa Iramba Mashariki Mwigulu Nchemba  akitoa tamko la kuwasailisha hoja binafsi bungeni katika kikao kijacho,alipozungumza na waanshishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,ambapo ataitaka Serikali kuanzisha mfuko wa Elimu wa vyuo vikuu,kulia ni Katibu wa Mbunge Kwagilwa



“Serikali ina mzigo wa kugharimia elimu ya juu kwa bajeti ya Serikali inayoumiza idara zingine za wizara kwa mfano, takribani asilimia 80 ya matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2012/13 ilielekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu,”


MBUNGE wa  Iramba Magharibi kupitia  CCM, Mwiguli Nchemba, amesema atapeleka hoja binafsi katika kikao cha Bunge lijalo  kuitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria, wa kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Juu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Nchemba alisema hoja hiyo ina lengo la kuwezesha kuundwa kwa chombo hicho muhimu ambacho   ikiwezekana kipewe hadhi ya kibenki ili kiwe na uwezo wa kisheria katika ufuatiliaji wa madeni ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Serikali ina mzigo wa kugharimia elimu ya juu kwa bajeti ya Serikali inayoumiza idara zingine za wizara kwa mfano, takribani asilimia 80 ya matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2012/13 ilielekezwa kwenye mikopo ya elimu ya juu,”alisema Nchemba.
Alisema mfuko huo utasaidia  kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato na mfumo wa kukopesha wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia taasisi za kibenki na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zitakazowezesha  kumkopesha kila mwanafunzi aliyepata nafasi ya kujiunga na elimu ya juu kwa asilimia 100.
“Msingi wa hoja yangu ni madhara yanayojitokeza kutokana na mfumo wa utoaji wa mikopo unakwamisha nia njema ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ya kutoa elimu ya juu kwa Watanzania wengi hususan watoto wa maskini.”alisema.
Nchemba alitoa mfano kwamba takwimu zinaonyesha mwaka 2004/05 zilitumika zaidi ya Sh22 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 16,345 kwa kiwango cha Sh2,500 kwa siku, mwaka 2005/06 kwa  wanafunzi 42,729 zilitumika takribani Sh56 bilioni.
Alisema mwaka 2011/12 zilitumika takribani Sh320 bilioni  kwa ajili ya wanafunzi 94,073 kwa kiwango cha Sh7,500 kwa siku na kwamba ifikapo mwaka  2015/16 tutahitaji zaidi Sh500 bilioni kwa wanafunzi 140,000 kitu ambacho kinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
“Wizara zinazosimamia moja kwa moja Rasilimali za Taifa mfano Maliasili na Utalii, Nishati na
Madini, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mifugo na Uvuvi zipangiwe kiwango cha fedha za kuchangia kwenye mfuko wa elimu ya juu kila mwaka ili kusaidia kutunisha mfuko huo.”alisema na kuongeza;
“Mikopo yote itozwe riba na kiwango cha riba kiwe sawa gharama ya ukopaji kwa Serikali. Hii itasaidia kulinda thamani ya mkopo na kusaidia mkopo usiolipwa kuongezeka kwa kiwango sawa na kile cha uuzaji wa dhamana za Serikali.”
back to top