KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema baadhi ya makada wa chama hicho, ni mitambo ya kupika majungu hali ambayo inaendeleza makundi.
Kinana alisema hayo juzi wakati akizungumza na
viongozi wa chama hicho na wananchi aliposimama kwa muda mkoani hapa,
akiwa safarini kuelekea Kigoma ambako atafanya kazi mbalimbali za jamii,
ikiwa ni maandalizi ya sherehe za kutimiza miaka 36 ya CCM
zitakazoadhimishwa Jumapili ijayo.
“Kuna baadhi ya makada ambao kazi yao ni
kuwagombanisha viongozi wao kwa kupikiana majungu, wapo wanaodiriki
kutuma hata ujumbe wa simu za mkononi kwa mwenyekiti wa chama kumweleza
kuwa katibu fulani hafai,” alisema Kinana.
Alisema fitina hizo zikiendelea zitakidhoofisha
chama na kwamba, wenye malalamiko wanatakiwa kuyatoa kwa viongozi wao
siyo kuruka kwenda ngazi za juu.
Pia, Kinana aliwataka viongozi kuwa makini kuna
watu wanaopika majungu kwa ajili ya kujipatia fedha, kwani hupika
majungu na kueleza mbinu watakazotumia kuwanusuru viongozi hao.
“Ili kukinusuru chama lazima wanaCCM tuache
majungu, hayajengi! Kiongozi unapoletewa majungu fuatilia ili kujua
ukweli, wenye majungu hawana nafasi kwenye ofisi yangu wanafahamu
nitawaumbua,” alisema Kinana. Alisema baadhi ya wapika majungu wanafanya
hivyo wakiwa na malengo binafsi, hasa uchu wa madaraka.
Alisema amefuatilia na kubaini muda mwingi ndani
ya CCM unatumiwa na makada katika malumbano kwa sababu za kupikiana
majungu, jambo ambalo alitaka likomeshwe na watakaobainikwa
watachukuliwa hatua za nidhamu. Kinana alisema huu siyo wakati wa
viongozi wa CCM kulumbana, bali kukijenga chama kiweze kutatua kero za
wananchi.
“Nimefuatilia na kugundua kuwa malumbano mengi
hayapo kwa malengo ya kutetea masilahi ya wananchi, bali ubinafsi na
uchu wa madaraka, tunasema hapana! Huu ni wakati wa kutambua tunatakiwa
kujenga chama chetu,” alisema Kinana na kuongeza:
“Vikao vingi vinavyofanyika sasa unakuta siyo
kuzungumzia jinsi ya kushughulikia matatizo ya wananchi, bali ni
kumshughulikia kada au kiongozi hali hii hatutafika ndiyo maana nasema
tunatakiwa kuwa wamoja kwa ajili ya kujenga chama chetu.”
Alisema zamani vikao vya chama viliitishwa kwa
mambo ya msingi ya kujadiliwa, lakini hivi sasa vikiitishwa vinakuwa vya
kushughulikia mtu.
“Binafsi wananijua sina muda wa kuhangaika na
mambo ya nani kafanya nini, maana kama nataka kufuatilia taarifa za
kiongozi najua utaratibu upi unafaa kujua kinachoendelea, siyo huu wa
kupewa taarifa tu na mtu,” alisema Kinana.