Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuzindua miradi minne ya ujenzi wa barabara na daraja mkoani Tabora leo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango, alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa pamoja na shughuli nyingine, Rais Kikwete leo ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi wa Daraja la Mbutu lililoko wilayani Igunga, mkoani humo.
Balozi Mrango alisema kesho Rais Kikwete ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara za Nzega–Puge, Puge–Tabora, Tabora–Ndono na Tabora-Nyahua, ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Alisema keshokutwa Rais Kikwete ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ndono hadi Urambo.
Alisema uzinduzi wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuhakikisha kuwa makao makuu ya mikoa yote yanaunganishwa kwa barabara za lami.
“Miradi hii ni mafanikio makubwa katika sekta ya usafirishaji na itatoa chachu kubwa kwa uchumi wa mkoa wa Tabora na Taifa kwa ujumla,” alisema Balozi Mrango na kuongeza:
“Miradi hii itasaidia katika kuimarisha usafiri wa barabara kati ya Tabora na mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Singida na Dodoma.”