
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Taifa, Abdallah Bulembo
HALI si shwari ndani ya Jumuiya ya Wazazi ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya Diwani wa Kata ya Magomeni, Julian
Bujugo kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiitaka
Jumuiya hiyo kumlipa Sh3 bilioni kama gharama alizotumia kukarabati
majengo ya Shule ya Sekondari Kaole iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Sekondari hiyo awali ilikuwa chini ya jumuiya
hiyo lakini baada ya kushindwa kujiendesha, ilichukuliwa na Bujugo
ambaye aliikarabati na kuibadilisha kuwa Chuo cha Kilimo Kaole, ambapo
huchukua asilimia 75 ya mapato huku asilimia 25 zikienda katika mfuko
wa Jumuiya hiyo.
Hatua hiyo imekuja siku tatu baada ya Mwenyekiti
wa Jumuiya hiyo Taifa, Abdallah Bulembo kumtaka Bujugo aikabidhi shule
hiyo kwa jumuiya kabla hajachukuliwa hatua za kisheria.
Katika maelezo yake, Bulembo alisema Bujugo hana
haki ya kuendelea na ujenzi wowote katika majengo ya chuo hicho kwa kuwa
mikataba aliyoingia na jumuiya ni feki na haina baraka za Baraza Kuu wa
Wadhamini la Wazazi, huku akifafanua kuwa diwani huyo alikabidhiwa
shule ili awe meneja lakini alikiuka makubaliano na kuifanya kuwa chuo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es
Salaam, Bujugo alisema kesi hizo namba 16 na 20 amezifungua juzi, ikiwa
ni wiki mbili tangu kupewa barua na jumuiya hiyo akitakiwa kusimamisha
ujenzi wa chuo hicho.
“Nimefungua kesi namba 16 ambayo inalenga kuizuia
jumuiya kutowasumbua wanachuo na kesi ya pili ni namba 20 ambayo
inawataka wanilipe gharama nilizotumia kukarabati chuo” alisema.
Alifafanua, “Niliingia nao mkataba ambao
tuliusaini mwaka 2010 kati yangu mimi, aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya
ambaye kwa sasa ni marehemu, Athumani Mhina pamoja na katibu ambaye
mpaka sasa yupo katika jumuiya, Khamis Dady” alisema Bujugo huku
akionyesha mkataba huo. Akifafanua fedha anazoidai jumuiya hiyo alisema
ili kuyaachia majengo ya chuo hicho, ameitaka jumuiya hiyo ya wazazi
kumlipa Sh3 bilioni kama gharama alizotumia kufanya ukarabati.
“Wakati wananikabidhi shule hii niliwakuta walimu
wanadai fedha na nikawalipa Sh45 milioni. Nimelipa madeni ya Mamlaka ya
Mapato (TRA)Sh65 milioni, umeme nilikuta wanadaiwa Sh15 milioni,
nilitumia zaidi ya Sh1.8 bilioni kufanya ukarabati wa majengo, ukiweka
na gharama nyingine inafikia Sh3 bilioni,” alisema Bujugo na kuongeza;
“Ninachotaka ni wao kunilipa gharama zinizotumia,
sina kinyongo na mtu na wala sitaki kuking’ang’ania chuo. Kwanza pale
chuoni kuna wanafunzi 300 wanashindwa kusoma kwa sababu ya mvutano huu.”
Akizungumzia kauli hiyo Bulembo aliliambia gazeti
hili jana kwa njia ya simu kwamba, msimamo wake uko palepale na chuo
hicho ni lazima kirudi mikononi mwa jumuiya hiyo.
“Nilishasema hata nilipokuwa wilayani Bagamoyo,
mikataba ile aliyoingia ni feki na lazima chuo kirudi mikononi mwa
jumuiya” alisema Bulembo.